Rwanda Leo
Image default
HABARI SIASA SLIDE

DRC: Kundi la Mayimayi wameamua kuweka silaha chini

Wapiganaji wa kundi la Maimai nchini Congo, wameitikia wito uliotolewa na rais wa nchi hiyo Felix Tshisekedi, wa kuweka chini silaha na kujiunga na jeshi la serikali au kurudi katika maisha ya kawaida.

Mamia ya wapiganaji hao kutoka kundi la UPCL wamejikusanya katika mji mdogo wa Kalunguta tayari kwa kusalimisha silaha zao.

Kulingana na meya wa mji wa Beni Bwanakawa Masumbuko Nyonyi aliyezungumza na BBC, hatua hiyo inatokana na wito wa rais wa taifa hilo Felix Tshisekedi wa kuwataka wapiganaji hao kuweka chini silaha mwezi wa Aprili mwaka huu.

Kulingana na meya huyo wito huo unatokana na mateso waliopitia wakaazi wa mji huo na viunga vyake mbali na mipango ya kuimarisha jeshi la taifa hilo ili kuweza kukabiliana na wapiganaji wa ADF ambao wametajwa kuwa maadui wakubwa wa serikali ya taifa hilo.

”Tangu rais wa DR Congo alipopita mjini Beni alitoa wito kwa wapiganaji wa Majimaji kuweka chini silaha kutokana na mateso walioyapitia wakaazi wa mji huo kufuatia uvamizi wa mara kwa mara wa wanamgambo wa ADF, baadhi yao wamekubali wito huo”, alisema.

Hatahivyo amesema kwamba ni kundi dogo la wapiganaji hao ambalo limekubali kuweka silaha chini ili kujumuishwa katika ujenzi wa taifa hilo ambalo baadhi ya maeneo yake yamekuwa yakikabiliwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa kipindi cha muda mrefu.

Huku akitoa wito kwa makundi mengine katika mji wa Beni kuiga mfano huo, Bwanakawa amesema kuwa baadhi ya wale waliokubali kuweka chini silaha watajumuishwa kwenye jeshi mbali na huduma nyengine za kitaifa huku wale wanaotaka kupelekwa nyumbani pia wakihudumiwa na kusafirishwa hadi makwao.

”Kila mtu ataulizwa aina ya kazi anayotaka kufanya au kujifunza iwapo ni ujasusi atapelekwa huko na kuna wale ambao watafunzwa kazi za mkono – kama huduma ya taifa. Kuna njia nyingi ambazo wakati watachukuliwa wataingizwa ili waridhike”.

Aidha amesema kwamba wapiganaji walio na umri mdogo walioshinikizwa kujiunga na jeshi kama vile watoto wadogo watawasilishwa katika mashirika yasiokuwa ya kiserikali ili kusaidiwa na baadaye kurudishwa nyumbani.

”Tunajua kwamba wanamgambo wa majimaji hawakuwa wakifuata sheria za kimataifa kwamba hawafai kuwapatia watoto silaha, hivyobasi kuna watoto walio na umri wa hata miaka 15 waliopatiwa silaha ili kujumuika katika vita, kitu tutakachofanya ni kuwachukua na kuwakabidhi mashirika yasiokuwa ya kiserikali ili kuwasaidia kabla ya kuwarudhisha nyumbani kwao”.

Meya huyo amesema kwamba jitihada za serikali ya DR Congo ni kuhakikisha kuwa wanasalia na adui mmoja ambaye ni wapiganai wa ADF.

 

@RwandaLeo

Maoni Husiano

Mombasa: Gavana Hassan Joho amewapeleka kotini wanasiasa 4

Leki Aimat

RWANDA: WABUNGE WA AFRIKA WALALAMIKIA SERIKALI

Leki Aimat

RWANDA: SHERIA ZA UKOLONI ZAPIGWA MARUFUKU

Leki Aimat

Toa maoni