Rwanda Leo
Image default
HABARI SLIDE

RWANDA: MAJENGO KWENYE MABONDE YAANZA KUBOMOLEWA

Mamlaka ya jiji kuu la Rwanda Kigali imeanza zoezi la kuharibu miundo mbinu iliyojengwa kwenye maeneo ya mabondeni jijini humo.

Hatua hii imefuatia agizo la serikali miaka miwili iliyopita kuwataka watu wanaoendeshea shughuli zao kwenye maeneo ya mabonde kuziondoa katika hatua ya kuhifadhi mazingira.

Ni zoezi lililoanzia kwenye wilaya ya Nyarugenge moja ya wilaya tatu za jiji la Kigali.Hatua hii imechukuliwa baada ya wenye miundombinu mbalimbali kukaidi miito ya serikali ya kuwataka kuhama bila mafanikio.

Bomoa hii haijapokelewa vema na waathirika huku baadhi yao wakihoji hatima yao. Mbarushimana Ibrahim ni mmoja wao ambaye nyumba yake ya biashara za baa kumbi za starehe kwa ujumla iliwekwa chini.

‘’Awali tulipata taarifa za maagizo ya mdomo tu hatukupokea barua yoyote ya maandalizi.Nimekuwa naendelea na shughuli zangu hata hivyo bila kujua mpaka wa kiwanja changu na eneo la serikali kwenye bonde hili,lakini sasa kufuatia zoezi hili nimeelewa ni wapi napaswa kukomea’’Alibaini Ibrahim

Shughuli za kubomoa majengo kwenye eneo hilo zimefanyika kwa mara ya kwanza mwezi mmoja baada ya muda uliotolewa kuisha.

Takwimu zinaonyesha kwamba tangu agizo hilo kutolewa miaka miwili iliyopita kazi hii imefanyika katika kiwango cha asilimia 2% tu

Ni kutokana na hali hii ambapo mkuu wa wilaya ya Nyarugenge Bi Kayisiime Nzaramba anasema hatua hii kama ilivyobainishwa hapo awali inalenga kulinda na kuhifadhi mazingira.

‘’Wananchi walikaidi mwito huu kwa sababu kila mmoja alikuwa anatoa hoja na sababu kuhusu uwekezaji wake huku wakisahau, kwamba waliweka huo uwekezaji kinyume cha sheria’’Alisema mkuu wa wilaya ya Nyarugenge

Shughuli ya kuondoa majengo na uwekezaji mwingine kwenye maeneo ya mabonde huenda ikaendelea kwa muda mrefu ikizingatia kwamba umbile la nchi la jiji la Kigali ni milima na mabonde.

 

@RwandaLeo

Maoni Husiano

Serikali kutumia nguvu kuwaondoa watu kwenye maeneo ya miteremko

Leki Aimat

RWANDA NI SALAMA-WAZIRI WA MASHAURI YA KIGENI

Leki Aimat

AFRIKA LAZIMA IWEKEZE KATIKA NGUVU KAZI-RAIS KAGAME

Leki Aimat

Toa maoni