Rwanda Leo
Image default
HABARI SIASA SLIDE

RWANDA: RAIS KAGAME AKIRI KUNA DOA KATI YAKE NA UGANDA

Rais wa Rwanda Paul Kagame amekiri kuna hitilafu katika uhusiano wa Rwanda na Uganda. Kwenye mahojiano yake na gazeti la The East African Rais Paul Kagame alisema sintofahamu inayoendelea kati ya mataifa hayo mawili mpaka sasa mzizi wake ni wapinzani wa Rwanda walioko  nchini Afrika Kusini ambao wameamua kuifanya Uganda kama kaka mkubwa wa kuwasaidia kuhatarisha usalama wa Rwanda.

Amesema kwa muda sasa watu hao(ambao hakuwataja majina) wamekuwa wakiishawishi Uganda kwa kutoa taarifa za uongo kuhusu Rwanda kwa lengo la kupata msaada wa nchi hiyo.

Kumekuwepo na taarifa kwamba kiongozi wa kundi la uasi la RNC linaloongozwa na Kayumba Nyamwasa mkuu wa zamani wa majeshi ya Rwanda aliyeko uhamishoni nchini Afrika Kusini linaendeshea harakati zake mjini Kampala Uganda.

Amesema taarifa zinazotolewa na watu hao  kwa bahati mbaya serikali ya Uganda imekuwa ikiziamini  hali ambayo imepelekea uhusiano huo kudorora.’’Baadhi ya taarifa zinazotuteta na Uganda kuziamini zinatolewa na watu hao walioko Afrika Kusini na ukifuatilia vema, watu hao wamekuwa wakiandaa harakati mbaya dhidi yetu huku wakitafuta msaada kutoka Uganda’’Alibaini Rais Kagame

Kwenye mahojiano hayo Rais Kagame alisema kwamba suala hili serikali za nchi zimelizungumzia karibu mara mbili bila mafanikio mpaka sasa.

‘’Tumezungumzia suala hili ndani ya miaka iliyopita, tunaweza kutatua tatizo hilo na likaisha ikiwa watu wataamua kutojipendelea au kupenda mambo yaende kombo’’ Alisema Rais Kagame

Uhusiano wa Uganda na Rwanda ni wa kihistoria kutokana na mapinduzi ya serikali zilizoko madarakani kwa sasa kwenye nchi hizo zilizokuwa na urafiki wa  chanda na pete. Rais Kagame anakubali kuwepo kwa historia nzuri ya nchi hizo na kukiri kwamba ni bahati mbaya nchi mbili kujikuta kwenye hali hii.

‘’Haingii akilini ukitazama historia baina yetu na msingi mzuri uliojengeka mpaka sasa kujikuta katika hali hii ambayo inaendelea hadi tunavyozungumza’’

Kwa upande mwingine kwenye  mahojiano haya alizungumzia pia uhusiano wa Rwanda na Burundi huku akibaini tatizo la Burundi ni la ndani na wala haifai litwike nchi nyingine.

‘’Ni tatizo rahisi,chukua mfano wakati Burundi ilipokuwa ikisema Rwanda ndiyo tatizo lake pekee watu walichukua maamuzi, na kwa mfano leo tuseme Rwanda haipo tena, ina maana Burundi haitakuwa na tatizo? Alihoji Rais Kagame.

Rais Kagame ambaye ni mwenyekiti wa sasa wa jumuiya ya Afrika mashariki amesema ana imani hatamu zake za uongozi  zitakwenda vema katika kipindi cha mwaka mmoja kama ambavyo mambo yalikwenda vizuri mwaka jana wakati Uganda ilipokuwa na uenyekiti wa jumuiya hiyo.

 

@Rwanda Leo

Maoni Husiano

Prof.Sam Rugege aomba wazalendo wa Nyagatare kuonyesha mikono yao ili rushwa imalizike

Leki Aimat

Rwanda:Bwana arusi amuacha mkewe kanisani akakimbia

Leki Aimat

MNACHUKULIANA NA WAJINGA KWA FURAHA

Leki Aimat

Toa maoni